KILIMO BORA CHA (KABICHI) CABBAGE

UTANGULIZI
Kabichi ni aina ya mbogamboga ambayo inatunga majani yake kwa kujiviringisha na kutengeneza mduara. Mboga hii inaweza kuliwa bila kupikwa au kuchemshwa kwa kutengeneza kachumbari. Pia inaweza kupikwa pamoja na vyakula kama vile nyama na maharagwe. Kabichi ni chanzo kizuri cha vitamin K, vitamin C na afya kiujumla

ASILI YAKE
Kuna ugumu kuelezea historia ya Kabichi, lakini ni zao ambalo liligundulika na lilikuwa likitumika Ulaya kabla ya miaka 1000 BC. Nchini Tanzania kabichi hustawishwa zaidi katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Morogoro, Tanga, Iringa na Mbeya. Kabichi ina madini aina ya chokaa, kambakamba, protini na maji kwa wingi.

HALI YA HEWA
Zao la kabichi hustawi  katika mwinuko kati ya mita 1200 hadi 1900 kutoka usawa wa bahari na hali ya ubaridi, pia Udongo ambao ni Tifutifu unaohifadhi unyevu kwa muda mrefu na una Rutuba nyingi na Usiotuamisha maji Usio na chumvichumvi nyingi.Kwa udogo wenye mbolea ya samadi huongeza uzalishaji kwa wingi.

AINA ZA KABICHI

  • Oxheart
    Kabichi zake ni ndogo zilizochongoka mfano wa moyo wa ng’ombe. Zinapendwa sana na walaji kutokana na ladha yake tamu. Hukomaa mapema na hazipasuki.
  • Early Jersey Wakefleld
    Aina hii inazaa kabichi zenye umbo lililochongoka kidogo (koniko) na zinazofunga vizuri. Kabichi moja inaweza kufikia uzito kati ya kilo 1.5 hadi 2.0. Hukomaa mapema (siku 90 hadi 100) tangu kupandikiza miche.
  • Prize Drumhead
    Vichwa vyake ni vikubwa (Kilo 2.0 mpaka 2.5) na bapa. Huchelewa kukomaa (Siku 110 hadi 120) tangu kupandikiza miche na hupasuka kirahisi. Aina hii huvumilia hali ya jua kali.
  • Copenhagen Market
    Vichwa vya Copenhagen Market ni vya mviringo na hupasuka kirahisi. Aina hii pia hukomaa mapema (siku 90 hadi 100) tangu kupandikiza miche.
  • Glory of Enkhuizen
    Vichwa vyake ni vya mviringo. Aina hii huvumilia hali ya juakali, lakinihuchelewakukomaa (siku 110 hadi 120) tangu kupandikiza miche na haivumilii hali ya kupasuka.
  • Aina nyingine ni Brunswick na Danish Ball head.

UTAYALISHAJI WA SHAMBA
Unaweza kutumia trecta, jembe la mkono au la ng’ombe kutayarisha shamba, shamba litayarishwe mwezi mmoja kabla ya kupandikiza miche kwa kukatua ardhi hadi kufikia kina cha sentimita 30. Lainisha udongo na tengeneza matuta. Weka mbolea za asili zilizooza vizuri kiasi cha ndoo moja hadi mbili, kwa eneo la mita mraba 10. Mbolea hii iwekwe katika kila shimo. Kiasi kinachotakiwa ni kilo moja au kopo moja la Tanbond kwa kila shimo. Hii ni sawa kuweka na tani 10 hadi 20 kwa hekta. Katika sehemu zenye upungufu wa madini ya fosiforasi mbolea aina ya N.P.K yenye uwiano wa 5:15:5 itumike. Kiasi kinachotakiwa ni kijiko kimoja cha chai chenye gramu 5 kwa kila shimo la mche.

UTAYALISHAJI WA MBEGU
Mbegu hutayarishwa kwa kuotesha kwenye kitaku kabla ya kupanda shambani, Andaa kitalu vizuri na weka mbolea za asili zilizooza vizuri kwa kiasi cha ndoo 5 – 10 za ujazo wa kilo 20 kwenye eneo la mita za mraba 10. Changanya na udongo kisha lainisha udongo kwa kuvunja mabonge makubwa kwa kutumia reki. Tengeneza tuta lililoinuka kwa sentimita 25 na lenye upana wa mita 1. Mwagilia maji kwenye tuta siku moja kabla ya kusia mbegu. Kiasi cha mbegu zinazohitajika ni gramu 1 kwenye eneo la mita 1 ya mraba hivyo hekta 1 huhitaji gramu 200 – 300. Sia katika umbali wa sentimita 15 toka mstari hadi mstari na kina cha nusu sentimita.Funika mbegu na udongo laini kasha tandaza nyasi kazu ili kuhifadhi unyevu.Mwagilia maji kila siku asubuhi na jioni mpaka mbegu ziote, huota kwa muda wa siku 5 – 10.

UPANDAJI
Upandaji wa Kabichi hufanyika kwa kupandikiza miche ambayo ipo tayari kwa kupandwa shambani, miche huwa tayari kupandwa baada ya wiki 3 – 5 tangu kusia kwa mbegu. Miche huwa na urefu wa sentimita 15 – 20. Ng’oa miche kwa uangalifu na pandikiza kama ilivyokuwa kitaluni na hakikisha mizizi haipindi wakati wa kupandikiza. Nafasi ya kupandikiza: Hutegemea aina ya kabichi – zenye vichwa vikubwa (Drumhead) ni sentimita 60 kutoka mche hadi mche na sentimita 75 toka mstari hadi mstari. – Zenye vichwa vidogo (Oxheart) ni sentimita 40 – 50 kutoka mche hadi mche na sentimita 60 toka mstari hadi mstari. – Umbali toka tuta moja na jingine ni sentimita 60. – Muda mzuri wa kuotesha ni asubuhi au jioni – Baada ya kupandikiza weka matandazo kama vile nyasi kavu ili kuhifadhi unyevu na kuzuia magugu kuota kwa urahisi.

MBOLEA
Mbolea ya kukuzia (S/A) huwekwa baada ya wiki 4 – 6 baada ya kupandikiza miche na kabla ya vichwa havijaanza kufunga. – Kiasi cha kilo 80 huhitajika kwa eka moja. – Kilo 40 ziwekwe baada ya wiki 4 – 6 na kilo 40 ziwekwe tena baada ya mwezi mmoja – Mche mmoja huhitaji kiasi cha kidogo cha gramu 5 – Mbolea iwekwe kuzunguka shina umbali wa sentmita 10 – 15 kutoka kwenye shina. Muhimu: Epuka kuweka mbolea nyingi, kwani husababisha vichwa visifunge vizuri (kabichi zinakuwa nyepesi)

UPALILIAJI & UNYEVU
Katika stajika kupalilia kwa makini kwa kupalilia juu juu ili kuepuka kukata mizizi ili zisizulike maana kabichi haina mizizi ya kina kirefu. Kuongeza matandazo husaidia kupunguza palizi a mara kwa mara. Ili kupata mazao mengi shamba linatakiwa liwe na unyevu wa kutosha, kama ni kipindi cha kiangazi inatakiwa umwagilie hata mara mbili kwa wiki.

MAGONJWA & WADUDU

MAGONJWA

  • Kuoza Shingo (Bacterial Softrot)
    Ugonjwa huu husababishwa na vijidudu vya bakteria ambavyo viko kwenye udongo. Hushambulia kabichi na kuzifanya zibadilike rangi, kuoza na kutoa harufu mbaya. Vijidudu vidogo vidogo pia huonekana kwenye sehemu iliyooza.
    Zuia ugonjwa huu kwa kuzingatia yafuatayo:-
    – Epuka kujeruhi kabichi wakati wa kuvuna
    – Vuna kabichi wakati hakuna mvua.
    – Usilundike kabichi kwa wingi na kwa muda mrefu.
    – Hifadhi kwenye sehemu yenye ubaridi na yenye kuingiza hewa ya kutosha
    – Ng’oa masalia, choma moto na lima shamba mara moja baada ya kuvuna.
    – Badilisha mazao.
  • Uozo Mweusi (Blackrot)
    Huu pia ni ugonjwa unaosababishwa na vijidudu vya backteria na hushambulia sana kabichi. Dalili kubwa za ugonjwa huu ni majani kugeuka rangi na kuwa ya njano na baadae kikahawia. Majani huanza kunyauka toka kwenye kingo zake na kuacha alama ya “V”. Kingo zinakuwa na rangi nyeusi isiyokolea. Baadaye majani yaliyoshambuliwa hudhoofika na kupukutika. Kama ukikata jani au shina, mviringo mweusi huonekana kwenye vena. Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kwa kuzingatia yafuatayo:-
    – Badilisha mazao kwa muda wa miaka miwili usipande kabichi najamii yake.
    – Panda kabichi kwenye sehemu ambayo haituamishi maji.
    – Kitalu na mazingira yawe safl daima.
    – Punguza miche ili kupunguza msongamano.
    – Ondoa masalia yote ya kabichi shambani baada ya kuvuna na yachome moto.
    – Panda mbegu zilizothibitishwa na wataalamu.
  • Kuoza Shina (Black leg)
    Ugonjwa huu chanzo chake ni ukungu. Dalili kubwa za ugonjwa huu ni kuwepo kwa madoa yaliyodidimia yenye rangi ya kikahawia kwenye shina karibu na usawa wa ardhi, ikifuatiwa na kuvimba kwa shina. Baadaye uyoga mweusi huonekana kwenye uvimbe huo. Pia uozo wa rangi ya kikahawia huonekana ndani ya shina. Kwenye majani huonekana madoa meusi ya mviringo yaliyozungukwa na uyoga mweusi. Zuia ugonjwa huu kwa kuzingatia yafuatayo:-
    – Panda katika sehemu ambayo haituamishi maji.
    – Badilisha mazao; kwa muda wa miaka mitatu usipande zao la kabichi na jamii yake
    – Lima shamba mara baada ya kuvuna ili kuwezesha masalia ya mazao kuoza haraka kabla ya kupanda.
    – OndOa kabichi zote zilizoshambuliwa shambani.
    – Tumia dawa za kuzuia magonjwa ya ukungu kama vile Ridomil.
  • Uvimbe wa Mizizi (Clubroot)
    Huu pia ni ugonjwa unaosababishwa na kuvu au ukungu. Hushambulia mizizi na dalili zake ni kudumaa kwa mmea na majam kukunjamana. Baadae mmea huoza.
    Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kwa kubadilisha mazao.
    •Madoajani Meusi (Black Leaf Spot)
    Chanzo cha ugonjwa huu ni ukungu. Dalili zake m kuonekana kwa madoa madogo ya mviringo yenye rangi ya njano kwenye majani. Baadae madoa haya huwa makubwa na hugeuka kuwa meusi.
    Zuia ugonjwa huu kwa kuzingatia yafuatayo:-
    – Badilisha mazao
    – Hakikisha shamba ni safi wakati wote.
    – Ikibidi tumia dawa za ukungu kama vile Copperhydroxide (Kocide),Copper Oxychloride (Cupro).
  • Ubwiri Vinyoya (Downy Mildew)
    Huu ni ugonjwa wa ukungu ambao hupendelea sana hali ya unyevunyevu na baridi kali na huonekana zaidi kwenye kitalu. Dalili zake ni majani kuwa na mabaka ya mviringo yenye njano upande wa juu. Baadaye mabaka haya hubadilika na kuwa na rangi ya zambarau iliyochanganyika na nyeupe upande wa chini wa majani.
    Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kwa kutumia njia zifuatazo:-
    – Kilimo cha kubadilisha mazao
    – Hakikisha udongo hautuamishi maji na kitalu ni kisafi wakati wote.
    – Nyunyizia dawa za ukungu kama vile Zineb, Dithane M – 45, Copperhydroxide (Kocide) na Copper Oxychloride, Topsin -M na Ridomil.
  • Kuoza Shina au Kinyawhi (Dampmg offor End Wire Stem)
    Husababishwa na ukungu na hushambulia miche michanga. Miche iliyoshambuliwa huonyesha dalili za kunyauka, baadae huanguka na kukauka. Miche mikubwa huonyesha dalili za kudumaa. Sehemu ya shina iliyokaribu na ardhi hulainika na kuwa na rangi ya kikahawia.
    Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kwa kutumia njia zifuatazo
    – Punguza miche kama imesongamana.

– Nyunyizia dawa za ukungu kama vile Dithane M – 45, Ridomil, Thiophanate (Topsin – M).

WADUDU

  • Viwavi wa Kabichi (Diamond Backmoth)
    Viwavi hawa huwa na rangi ya kijani kibichi na alama ya mstari wa kung’aa mgongoni, Nondo hutaga mayai chini yajani na baada ya kuanguliwa viwavi hula sehemu ya chini yajani na kuacha ngozi nyembamba mfano wa dirisha la kioo. Ni muhimu kuuwa viwavi kwa sababu ndiyo wanaoleta madhara makubwa.
    Wadudu hawa wanaweza kuzuiwa kwa kunyunyuzia moja ya dawa zifuatazo:- Nogos, Pennethrin, Dimethoate, Sevin W.P. na Sumicidin.
  • Inzi wa Kabichi (Cabbage Sawfly)
    Mashambulizi hufanywa na kiluwiluwi mwenye rangi ya kijani kibichi au bluu. Hula majani yote ya kabichi na kubakisha vena au vishipa vya majani.
    Inzi wa kabichi wanaweza kuzuiwa kwa kutumia dawa za Caibaryl (Sevin), Dimethoate (Dimethoate Sapa), Pennethrin, na Fenvalerate (Sumicidin).
  • Sota (Cutworms)
    Hawa ni funza wakubwa wenye rangi ya kijivu. Hupendelea kujichimbia katika udongo wakati wa mchana na kukata miche michanga karibu na usawa wa ardhi wakati wa usiku.
    Zuia wadudu hawa kwa kutumia majivu au dawa kama vile Carbaryl, Fenvalerate, na Deltamethrin (Decis) mara baada ya kupanda. Kama mche utakatwa, mtoe mdudu huyu kwa kumfukua na kumuua. Kisha pandikiza mche mwingine.
  • Vidukari au Wadudu Mafuta (Cabbage Aphids)
    Wadudu hawa ni wadogo sana wenye rangi ya kijani, nyeusi au khaki. Baadhi yao wana mabawa na wengine hawana. Hufyonza utomvu wa mimea na husababisha majani kubadilika rangi na kuwa meupe au njano iliyopauka. Mmea hudumaa na hatimaye hukauka.Wazuie wadudu hawa kwa kunyunyizia mojawapo ya dawa zifuatazo:- Fenvalerate, Dimethoate, Lambda – Cyhalothrin (Karate) na Dichlorvos (Nogos).
  • Minyoo Fundo (Root knot Nematodes)
    Hawa ni wadudu wadogo wanaoishi ardhini na ambao hawaonekani kirahisi kwa macho. Hushambulia mizizi na kusababisha kabichi kudhoofu na hushindwa kufunga vizuri. Mimea iliyoshambuliwa mizizi yake huwa na nundunundu.
    Wadudu hawa wanaweza kuzuiwa kwa kuzingatia yafuatayo:-
    – Utumiaji wa mbolea za asili kila msimu hupunguza kuzaliana kwa wadudu hawa.
    – Usipande kabichi mfululizo kwenye sehemu ile ile wala jamii yake kama vile kabichi ya kichina na kolifulawa, ila badilisha kwa kupanda mazao mengine kama vile mahindi, karoti, radishi na vitunguu.
    – Ondoa masalia yote shambani ambayo yanaweza kueneza wadudu hawa na yachome moto.
  • African Mole Cricket
    Hawa ni aina ya panzi ambao hujificha kwenye nyufa za udongo mchana. Hujitokezajuu usiku kwa kuchimba udongo kutumia miguuyambele. Wadudu, hawa huharibu mizizi na hula majani ya miche michanga.
    Zuia wadudu hawa kwa kutumia dawa ya Carbaryl. Changanya gramu 50 (vijiko vitano vikubwa vya chakula) vya dawa pamoja na kilo moja ya mchele, mtama au pumba za mahindi au ngano. Ongeza maji kidogo kwenye mchanganyiko huo na kisha mwaga kwenye njia wanazopita wadudu hawa.

UVUNAJI
Kabichi hukomaa katika siku 60 mpaka 210 tangu kupandikiza miche. Hata hivyo muda wa kukomaa hutegemea na aina ya kabichi. Uvunaji hufanyika kwa kukata shina sentimita 2 – 3 kutoka kwenye kichwa kwa kutumia kisu. Ondoa majani ya nje na acha majani 2 au 3 ya kijani kwa ajili ya kuzuia kabichi zisikwaruzike na kuoza wakati wa kusafirisha. Punguza urefu wa majani ili kurahisisha ufungaji. Ni muhimu uvunaji ufanyike asubuhi au jioni. Ondoa kabichi zilizooza au kuharibika wakati wa kuvuna, kisha panga zilizobaki kufuata daraja kama vile ndogo, za kati na kubwa. Mavuno:- Kiasi cha tani 40 au zaidi za kabichi hupatikana kwa hekta moja kama zao limetunzwa vizuri.

Contact/ Wasiliana nasi 

Phone (Simu): +255766797400                                          Email: daudilyela@yahoo.com

Maisha Daily LogoOur Services ( Huduma zetu): 

  1. Research( Utafiti),

  2. Drip Irrigation Installation (Ufungaji wa Umwagiliaji wa Matone)

  3. Project Proposal ( Mapendekezo ya Miradi),

  4. Business Plan ( Plani za Biashara),

  5. Profit Assessment ( Upimaji wa Faida)

  6. Agricultural Books (Vitabu vya kilimo)

 

Leave a comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.